Dunia yaigeukia Tanzania. Makala ya: The Light Team

Dunia nzima sasa yaigeukia Tanzania.
Hii ni baada ya ugunduzi wa moja kati ya madini adimu sana duniani. Ugunduzi wa gesi aina ya helium katika bonde la ufa Tanzania.
Kwa kipindi kirefu sasa wanasayansi na watafiti mbalimbali walitaadhari dunia juu ya uwezekano wa kuisha kwa gesi ya helium hadi ifikapo mwaka 2030. Ni moja kati ya hatari kubwa sana kuwahi kutolewa, kwani madini haya yana mchango mkubwa sana katika maisha ya mwanadamu.
Gesi ya helium hutumika kwenye mambo mengi sana ikiwemo matumizi ya viwandani kuratibu na kuendesha mashine, matumizi katika vifaa vya matibabu kama mashine za MRI; na matumizi mengine mengi sana kama utakavyoweza kusoma katika vitabu na mtandaoni; vile vile utafahamu kwa upana matumizi ya madini haya. Pia unaweza kufahamu zaidi kuhusu thamani ya madini haya; kwa mahesabu ya haraka kwa kiwango cha madini yaliyogundulika mpaka sasa; thamani yake ni matrilioni ya fedha (nimetumia takwimu za uuzaji wa Helium za mwaka 2014 ambazo cubic meter iliuzwa kwa $3.43).
Serikali mbalimbali duniani zilishaingia katika kipindi cha dharura kukabiliana na upungufu wa gesi hii, Marekani, Uingereza, Urusi, China na mataifa mengine makubwa yalishaingia katika mkakakati mpya wa dharura wa matumizi ya gesi hii katika shughuli zao za viwanda, matibabu na Jeshi. Wanasayansi nao kutokana na uhitaji mkubwa wa gesi hii katika tafiti zao mbalimbali, walishaingia katika kipindi cha dharura kujiandaa na kuisha kwa gesi hii kwa mujibu wa makadirio ifikapo mwaka 2030.
Tanzania; Nchi yenye Neema pengine kuliko nchi yoyote ile duniani. Kwa mara nyingine tena yageuka tumaini la dunia na vizazi vijavyo. Hellen Briggs Mwandishi wa BBC akiripoti juu ya ugundizi wa gesi hiyo, amesema zaidi ya Lita trillion za helium zimegundulika katika bonde la ufa Tanzania. Ugunduzi huo uliotangazwa katika kongamano moja lijulikanalo kama Goldschmit Geochemical Conference, ni ugunduzi mkubwa zaidi uliowahi kutokea wa gesi hiyo. Ugunduzi huo umethibitisha kuwa gesi hiyo itaweza kutosheleza mahitaji ya dunia kwa miaka na miaka.
Ni kwa mara ya kwanza watafiti hao wamegundua gesi hii kwa malengo, kwani; mara nyingi gesi hii hugundulika kwa bahati tu pindi wafanyapo tafiti kuchunguza madini mengineyo. Kwa mujibu wa wanasayansi, gesi hii ipo kwa wingi sana katika mfumo mzima wa sayari zote, ila katika dunia yetu, gesi hii hupatikana kwa nadra. Vile vile ni aina ya gesi ambayo haiwezi kutengenezwa kwa njia nyingineyo yoyote ya ki-artificial.
Ni dhahiri kwamba dunia nzima itaigeukia Tanzania kama tumaini la madini haya kwa vizazi vijavyo. Ni fursa kubwa kwa taifa lenye hali duni sana kiuchumi. Hii inatuacha watanzania kama CEOs wa kuamua nini hatma ya nchi yetu kwa fursa hii mpya iliyojitokeza. Swali ni kwamba, Je; Watanzania wanafahamu kuhusu ugunduzi huu? Lakini pia wako tayari kutumia fursa hii kupanda viwango vya kiuchumi, kisayansi na kimaisha? Unajua kwamba wewe ndio muamuzi, na kinachoamua ni uwezo wako wa kuiandama na kuitumia fursa hii? Ma geologist wetu wapo tayari kulitumikia taifa kwa kuhakikisha gesi hii inavunwa ipasavyo? Je Tunao wa kutosha? Kama hatuna tunafanya nini? Vipi kuhusu viongozi? Tunao wenye moyo wa dhati wa utumishi wa Taifa letu katika ngazi za kiserikali, kitaasisi mpaka kijamii? Au tunao wananchi ambao wao ni wazuri wa kusubiri nchi kufeli na viongozi waliowachagua wao wenyewe kukosea ndipo walalamike?
Ni maswali ya msingi sana ya kujiuliza kabla hatujakimbilia kwenye kuuza gesi kwa pupa. Kwa nini tusiwe na turning point ya ukoloni mamboleo! Tumeona wazungu wanakuja tunawapa madini, haooo wanasepa nayo, tumeona wachina wanakuja tunawapa bandari za bagamoyo wanapiga tu, wahindi nao wanarithishana tu migahawa huku mjini, migahawa iliyojengwa kwenye ardhi yetu bila ya kulipa kodi stahiki kama wawekezaji wasio wazawa.
Ugunduzi huu binafsi unanikumbusha ugunduzi wa rasilimali nyingi za kipekee zilizowahi kutokea Tanzania, Madini kama Tanzanite, dhahabu, mafuta, Ugunduzi ambao ulitoa tumaini kubwa kwa hatma ya maendeleo ya Nchi yetu. Tanzanite, Dhahabu, na uchimbaji mwingine ambao kwa miaka zaidi ya 30 umekua ukiipa Tanzania asilimia tatu tu ya mapato yake; achilia mbali soko bandia (black market) ambalo limeruhusu madini kusafirishwa bila ya kodi stahiki na hatimaye mawe yetu kutumika kutengenezea bidhaa ambazo mwisho wa siku zinaletwa tena kwetu kwa bei ya Mara 10 zaidi ya thamani ya dini lililotumika kutengenezea bidhaa hiyo. Huku ni kujiua na kuua watoto na watoto wa watoto wetu. HII NDIO MAANA HALISI YA UMASKINI.
Hata maana ya UMASKINI tume-define-niwa na wazungu. Ila UMASKINI maana yake ni nini? Chukulia uhalisia huu: wewe ni Mtanzania, una uhalali wote wa Utanzania, Je? Hii inakufanya uwe mrithi halali wa rasilimali hizi? Jibu langu ni NDIO (sijui lako). Sasa kama wewe ndio mwenye mali ya Tanzania, Iweje uitwe maskini! HAKUNA MTANZANIA MASKINI kwa kigezo cha mali. Ila watanzania ni MASKINI kwa vigezo vifuatavyo:
1.    Uwezo wa kutumia rasilimali zao wao wenyewe + Uwezo wa kujiamini na kuwaamini Watanzania wenzao
2.    Ufahamu kuhusu sisi ni nani, misingi ya maendeleo, taifa linahitaji nini, na dira ni ipi.
3.    Uzalendo wa kuijenga Nchi kwa kufanya kazi kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo; kila mtu anataka kula na hakuna anayetaka kujenga! (oow sorry, wachache wanataka kujenga)
Hayati Baba wa taifa Mwalimu JK Nyerere aliwahi kusema: Kama watanzania hawajaweza kutengeneza uwezo na miundombinu ya kutumia rasilimali zao kwa manufaa yao wenyewe na watoto wao, basi ni bora rasilimali hizo ziachwe mpaka watakapojijengea uwezo (niongeze na MOYO) wa kufanya hivyo.
Naamini ni wito wetu sote kama Watoto wa Tanzania, kwa serikali na wizara husika, Kwa taasisi za kielimu na taasisi kama familia; kwa watu binafsi kama mimi na wewe na yule; kuanza kuutazama ukombozi wa Taifa la Tanzania kwa mtazamo mpya. Hili taifa linatuhitaji sote, linahitaji kujitoa na kutumika. Tukiendelea kufanya mambo katika AKILI ZA NJAA NA UMASIKINI, tutauza kila kitu tulicho nacho kwa mataifa ya magharibi. Mwisho wa siku tutakapokosa vya kuuza kwa wa-magharibi tutajiuza na sisi wenyewe kuwa watumwa wao.
Kwa hali ya kufanya mambo bila kutazama hatma ya vizazi vijavyo, kuna hatari kubwa sana ya ukoloni kurejea tena Afrika kwa mara ya tatu, pengine karne kadhaa zijazo watoto wetu watatuma maombi ya kuwataka wa-magharibi waje kuwasaidia kuendesha mambo yanayohusu maisha yao wenyewe. Itakua aibu kubwa sana kwetu, tutakaokua tumekufa kwa wakati huo na fedheha kubwa kwa vizazi vyetu vitakavyokua hai kwa wakati huo.

UONGOZI NI MIMI, WEWE NA YULE. UONGOZI NI FIKRA NA MOYO UNAOJIJENGEA WA KUJITOA MUHANGA KUTUMIKA. UONGOZI NI VITA DHIDI YA UJINGA, UMASKINI NA MARADHI; UONGOZI NI KUZALISHA, UONGOZI NI KUFANYA MAAMUZI MAGUMAGUMU KWA MANUFAA YA VIZAZI VIJAVYO
Share on Google Plus

About The Light

0 comments:

Post a Comment