Saikolojia Ya Ukuaji wa Mtoto (Sehemu ya 2) na Frazier


MAENDELEO YA MTOTO

Maendeleo tutakayozungumza katika makala yetu ya leo ni yale yanayohusiana na mabadiliko au ukuaji unaotokea kwa watoto. Maendeleo haya hutazamwa tangu mtoto anapokua kichanga hadi utu uzima! Kwa kujifunza kuhusu maendeleo kwa mtoto, utaweza kutengeneza utaratibu Fulani wa kuorodhesha ili ikusaidie kufahamu ni nini au kipi watoto hufanya katika umri Gani. 

Kwa mfano; utajifunza kwamba watoto wenye umri wa miaka miwili hupenda kukimbia kimbia; hivyo inatakupasa uandae nafasi nzuri ndani kwako au nje ili waweze kupata nafasi ya kukimbia kimbia vizuri. Vile vile utajifunza kwamba watoto wenye umri wa miezi kadhaa Karibu na mwaka mmoja, hupenda kuweka kila wanachokishika mdomoni. Kufahamu hili kutakusaidia kuhakikisha kwamba vitu vyote mtoto anavyochezea viko katika hali ya usafi.

Kwa kukosa kufahamu kua ndivyo saikolojia ya ukuaji wa mtoto ilivyo kwa umri huo, wazazi na walezi wengi huwanyang’anya watoto wao vitu wanavyoweka mdomoni au kuwakaripia kwa kuwakataza. Ni kosa kufanya hivyo. Kama ni mzazi au mlezi kazi yako ni kuhakikisha kua vitu hivyo anavyochezea vipo katika hali ya usafi.

Saikolojia ya maendeleo ya mtoto ni moja kati ya maenea ambayo watafiti wengi huwekeza haswa kwa miaka ya karibuni. Mara kwa mara watafiti hugundua mambo mapya yahusuyo vile ambavyo watoto hukua, huendelea, na hujifunza.

Ni jambo jema kujifunza kupitia wataalam mbalimbali waliobobea kwenye fani hii, kwani mambo mengi mapya yahusuyo saikolojia hugunduliwa kila mara. Kujifunza Si lazima uwe shuleni au chuoni au uwe unatafuta cheti. Elimu ni maisha ya kila siku.

Tutazame Maeneo Ya Msingi Maendeleo Kwa Mtoto Hutokea

Tunaweza kugawanya katika maendeleo haya katika makundi matatu ili kujifunza maeneo haya kirahisi. Eneo la Kwanza ni Maumbile ya Nje (Physical Development) Eneo la Pili Ni Akili na Ufahamu (Cognitive) na Tatu ni Hisia na Mahusiano (Social and Emotional Development). Kugawanya hivi itatusaidia kujifunza.

Maendeleo Ya Kimaumbile (Physical Development), hutokea kwa kulandana na muda, ni rahisi pia kugundua kadri muda au miaka inavyozidi kusogea. Hii hujumuisha mabadiliko kwa kuongezeka upana na urefu wa mifupa, misuli n.k yote haya tunayajumuisha huku. Wenye elimu ya baiolojia wanajua zaidi, mnyambuliko wa hatua hizi.
Katika hatua hii ndipo pia maendeleo ya mtoto yanayohusiana na Maumbile huanza kutokea na kustawi, kwa mfano kutambaa, kutembea, kuandika n.k ni matokeo ya maendeleo ya maumbile ya mtoto. Kwa ufahamu wa haraka bila shaka hii itatutosha! Ila kwa wanaopenda kwenda kwa undani zaidi wanaweza kusoma kuhusu "Gross-motor development" na "Fine-motor Development".


Ni vyema pia tukitambua ya kua mazingira mtoto alipo huweza kuathiri kwa namna chanya au hasi maendeleo ya maumbile na matokeo ya maendeleo ya maumbile ya mtoto. Kwa mfano kukosa au kupata mlo kamili na wa kiasi cha kutosha, kupata au kukosa vifaa vya kujifunzia vya mtoto; (wazazi na walezi wataelewa kua wakati mwingine inawabidi wanunue vigati vya mtoto kushika na kujifunzia kutembea, au kupanga sebule kwa namna ambayo mtoto ataweza kujishika na kutembea).

Eneo la pili ni Maendeleo ya Akili na Ufahamu: Hili ni moja kati ya eneo muhimu sana kulifahamu. Wataalamu hupenda kuliita (cognitive development) au (Intellectual development). Hii ni hatua za mtu katika kupata ufahamu (process use to gain knowledge). Hili eneo linabeba maendeleo ya Lugha, Fikra, Mawazo, imagination, yote haya hujumuishwa katika kundi hili.

Lugha na Fikra kama nilivyotangulia kundika, ni matokeo ya maendeleo ya Akili na Ufahamu, na mambo haya mawili yana uhusiano wa Karibu sana, vyote vinahitajika kwenye Kupanga/Mipango, Kumbukumbu, Na Kutatua Matatizo (Planning, Remembering, and problem solving). Kwa kadri Watoto wanavyozidi kukua na kupata uzoefu juu ya Dunia waliyopo, Ujuzi huu (Kupanga/Mipango, Kumbukumbu, Na Kutatua Matatizo) hukua na kukua zaidi. 

Eneo la Tatu ni Maendeleo ya 'Kimahusiano na Kijamii' na Maendeleo ya Hisia (social-emotional development); Mambo haya mawili yamejumuishwa kwa pamoja kwa sababu yana uhusiano wa Karibu sana. Kujifunza namna ya kuhusiana na wengine ni maendeleo katika mahusiano na kijamii. Maendeleo ya kihisia kwa upande mwingine inahusisha hisia na uwezo wa kueleza hisia zako. Hili eneo pia ni muhimu sana na binafsi huwa napenda kulijifunza na kulijua zaidi katika upana wake.

Kuamini au Kujiamini, Woga, Ujasiri, Kiburi/Kujisikia, Urafiki, Utani, vyote hivi vipo katika kundi hili la Maendeleo ya Kihisia na Mahusiano na Kijamii. Mambo mengine ni pamoja na Aibu, Interest, na raha (kitu gani hukupa raha zaidi/pleasure).

Kujifunza namna ya kuonyesha hisia zako huanza tangu awali pindi ukiwa mdogo. Labda tuongelee mfano halisi ambao wote tutaweza kuelewa. Kuna watu ambao wana aibu sana kumueleza Binti kua wana hisia za kimapenzi kwake, anaweza akajipanga kumueleza binti kwa muda wa mwezi mzima na bado akifika atatetemeka na jasho litamtoka kila mahali! 

Hii ni hali ambayo imetengenezeka tangu akiwa mdogo! Hakuwa na uhuru na hakujengewa ujasiri wa kujieleza na kueleza hisia zake. Mfano mwingine, kuna mwanafunzi utakuta mwalimu akitaka kumchapa, atahoji kosa lake na pengine ataomba kujieleza; ila mwingine hatazungumza kitu ila atalala chini au kunyoosha mkono yaishe. Hizi ni hali ambazo zimejengeka katika mzizi wa hili eneo tulilolizungumzia hapo juu. Inakua imeanza tangu zamani sana.

Kama wewe ni mzazi au mlezi ni vyema sana ukawa unampa mtoto nafasi ya kueleza hisia zake na umsikilize pale anapojieleza. Mtie moyo awe mwepesi kueleza hisia zake. Kuna kitu katika saikolojia kinafahamika sana kama "self-concept" (vile mtu anavyojichukulia na kujijua) na "Self-esteem" (vile mtu anavyojithamini na kujikubali). Mambo haya mawili hutengenezwa sana na hatua hii ya maendeleo ya mtoto.


Ni muhimu sana kuwa na ufahamu wa haya mambo. Kwa mfano kwenye eneo la kwanza la physic na eneo la pili la Akili na ufahamu; mtoto anapoona ameweza kujifunza kutembea, kukimbia, kucheza mchezo Fulani, kuandika, anapoweza lugha; inamjengea ujasiri (confidence) na hii inapelekea mtoto kujikubali na kujielewa na pia kukuza hisia za kujipenda na kujithamini, kupenda kitu na kukithamini pia. (a healthy self-concept and sense of worth).

Maendeleo kwenye Maumbile ya nje, Akili na Ufahamu, Hisia na Mahusiano ya Kijamii kwa mtoto ni mambo ambayo yana uhusiano wa Karibu sana, na hutegemeana kwa ukaribu sana. Maendeleo kwenye eneo moja hupelekea maendeleo kwenye eneo jingine.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala haya na makala nyinginezo nyingi kupitia blog: lighttz.blogspot.com Tufuatilie katika ukurasa wetu wa Facebook “facebook.com/thelighttz” unaweza ukaacha comment zako hapo au kutuandikia barua pepe kupitia the.light.tz@gmail.com 

Hongera kwa kujifunza na Asante.
Share on Google Plus

About The Light