Saikolojia Ya Mtoto, Maendeleo Na Ukuaji - Frazier Light

Kusoma na Kuelewa juu ya ukuaji na maendeleo ya mtoto ni jambo muhimu sana katika kumlea na kumfunza mtoto. Hakuna mtoto anayefanana na mwingine katika saikolojia na hata ukuaji pia. Watoto hutofautiana katika maumbile(physical), ufahamu na kufikiri (cognitive), hali ya kuhusiana na wengine (social), na hata hisia (emotional growth).

Utashangaa kujua kua hata mapacha amabao wana vinasaba mfanano (having the same genetic makeup) hawafanani kila kitu, hususani kwa vigezo nilivyoorodhesha hapo juu. Mapacha huweza kutofautiana katika namna ya kujihusisha kimichezo, mmoja anaweza akawa anapenda sana mpira wa miguu na akisikia; “twende tukacheze mpira wa miguu” basi hukimbia upesi uwanjani ilihali mwenzake akiwa hana hamu au mvuto na mchezo huo au mchezo mwingine wowote.

Kurwa anaweza akawa mpenda vibinti sana ila doto akawa si mtu wa hayo mambo kabisa. Mfano mwingine pacha mmoja anaweza akawa anahusiana sana vizuri na watu au majirani ila mwingine akawa hana au hapendi sana kuzoeana na watu. Hii ni tofauti iliyopo kati ya mtoto na mtoto na kuna uwezekano kukua hata kufikia utu uzima na tabia hizi au zifananazo na hizi.

Unapopata ufahamu kama huu, unakusaidia sana; si tu kuelewa tofauti kati ya mtoto na mtoto au ukuaji wa baina ya mtoto mmoja na mwingine bali unakuwezesha pia kujua namna gani ya kuwalea katika namna ambayo haitaathiri ukuaji wao kimwili, kiakili na hata kisaikolojia.
Malezi ni magumu sana kama mzazi au mlezi anakua hafahamu hata kidogo maendeleo na saikolojia ya mtoto. Mahudhurio ya kliniki huweza kukupa ufahamu mzuri juu ya ukuaji na maendeleo ya mtoto kama utafanikiwa kumpata mtaalamu wa mambo haya.

Hebu fikiri juu ya watoto wanne au zaidi unaowafahamu. Utakubaliana na mimi kuwa baadhi huonekena kua na nyuso za furaha wakati wote, Baadhi huwa na personality nadhifu ila wengine hawako nazo nadhifu. Watoto wengine ni wachangamfu ila wengine ni wapole sana. Unaweza ukakubaliana na mimi pia kuwa watoto wengine ni rahisi kuwapenda ikilinganishwa na wengine.
Kuwasaidia au kuwalea watoto hawa wa aina tofauti tofauti huna budi kufahamu ngazi (sequence) za maendeleo ya mototo. Ufahamu juu ya maeneo ya ukuaji wa mototo ni muongozo mzuri katika malezi ya mtoto. Bila shaka tutaendelea kuwa pamoja katika mfululiza wa masomo haya kadri tutakavyowaletea katika blog hii yetu “lighttz.blogspot.com”.

Sambamba na haya tutajifunza pia juu ya maendeleo ya ubongo wa mototo na itakusaidia sana katika malezi. Bila shaka kila mzazi hupenda kuona mototo wake akifanya vizuri katika mambo yote, masomo, michezo, kazi, usikivu, n.k

Maendeleo yoyote ya ubongo wa binadamu hutokana na maendeleo chanya ya tabia/mwenendo wa binadam. Kuna uhusianao wa moja kwa moja (a direct influence) kati ya Ubongo na Tabia/mwenendo wa mtu. Mtu yeyote mwenye mwenendo chanya hutoa fursa ya ubongo kufahamu kwa urahisi, na kuendelea katika kujifunza na uwezo mkubwa katika kufanya kazi.


Stimuli chanya ni mambo ya msingi sana kwa maendeleo ya ubongo(positive stimuli are major factor in brain development). Kwa hivyo NI JAMBO LA MUHIMU/MSINGI SANA SANA SANA KWA MTOTO KUWA NA WAZAZI/MZAZI AU MLEZI MWENYE UPENDO WA DHATI. Watoto wadogo wanahitaji utegemezi na uhusisano wa kuaminika (young children need dependable and a trusting relationship); Na hii ni kwa sababu watoto hustawi sana katika mazingira ambayo ni predictable na nurturing (nimekosa Kiswahili cha haya maneno mawili) {Children thrive in environments that are predictable and nurturing}.

HITAJI LA USALAMA KWA KILA MWANADAMU NI LA KISAIKOLOJIA

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia Abraham Maslow, alisema, Hitaji la mwanadamu la usalama ni lazima litimizwe kabla ya ukuaji na maendeleo kutokea katika maeneo mengine. Akimaanisha Hitaji la usalama ni muhimu au ni la msingi na la mwanzo sana kufikiwa kabla ya mwanadamu huyu kuendelea na kukua katika mambo mengineyo. Utakubaliana na mimi kwamba ni kweli kua kama huhisi salama katika eneo au watu ulionao ni vigumu sana akili yako kuwaza na kutoa nafasi kwa mambo mengine kuendelea. (Safety must be met before growth and development occurs in other areas)

Na hili ni suala LA MSINGI SANA KWA WATOTO PIA. Hii inamaanisha nini kwa kwa walimu na walezi/wazazi? INAMAANISHA; Kuwa makini kutambua ni nini chaweza au humfanya mtoto au watoto unaowalea au/na kuwafundisaha wahisi KUOGOPA au KUTOKUA SALAMA.
Kuna wakati mtoto huweza kukukimbilia na kukukumbatia, ni kwa sababu anaamini kwako yuko salama. Nakumbuka nilivyokua mdogo, nilikua naogopa sana mbwa, na hadi leo mimi naogopa sana mbwa, mpaka imenijengea hali ya kuwachukia! (point muhimu: WOGA HUZAA CHUKI- Ukimfanya mtu akuogope kadri muda unavyozidi kwenda atakuchukia na kuzidi kukuchukia. Huwezi kupenda kitu na ukakiogopa na huwezi kuogopa kitu na ukakipenda).
Nilikua nikiona mbwa kama niko na mama yangu namkimbilia mama yangu na kumrukia kwa woga sana na kisha hunikumbatia na kuniambia USIOGOPE, HAKUNG’ATI. Hapo ndipo akili yangu ilipotulia tena. Na kama siko na mama yangu basi ujue nitakimbia na kupiga kelele mpaka nikute mtu mzima nimueleze anisaidie.

Ila siku hizi inaniumiza sana kuona haswa uswahilini mtoto anakimbizwa na mbwa halafu akimkimbilia mama yake au baba yake anaambulia Kipigo tena. Kwamba “kwa nini unachokoza mbwa, koma kabisa” Wazazi na walezi wa namna hii hawajui madhara ya wanachomwambia huyo mtoto. Madhara yake huja kuonekana darasani, au mtaani, au ukubwani; akiwa anaanza kujitegemea. Ndipo mzazi anaanza kutafuta mchawi!

Hivi vitu huchangia sana aidha kwa namna hasi au chanya ukuaji na maendeleo ya mtoto, Kwa mfano umewahi kucheza na mtoto labda wa miaka 3, 4 au 5 hivi halafu ukajikuta anakung’ata au anakupiga au akakutemea mate? Haya na mengine ni matokeo ya mambo niliyoandika na tuliyojifunza hapo juu. Au unakuta mtoto akiona wageni anang’ata vidole na kujishika shika na mama yake au baba yake huku akiona aibu sana au woga kuongea? Haya yote tutazidi kujifunza kwa kadri tutakavyoendelea.

Moja kati ya swali ambalo nataka ubaki nalo ni kwa nini watoto wa Wenzetu wanaoishi Dunia ya kwanza (first world countries) au nchi zilizoendelea, awe mweusi au awe mzungu, anakua mwepesi sana kufanya ugunduzi wa mambo ukilinganisha na huku kwetu Afrika? Je, sisi tumeumbiwa ubongo robo na wao wakapewa Kamili? Kwa nini sisi hatugundui sana mambo hususan kipindi hiki, kwa sababu zamani mababu zetu walikua wagunduzi. Waligundua moto, wakagundua silaha, michoro, dawa, n.k. Nikuache na Hilo. Unaweza kutujibu kupitia ukurasa wetu wa Facebook (facebook.com/thelighttz) au ukatutumia email (the.light.tz@gmail.com)

Kwa gharama yoyote mlee mtoto wako katika namana ambayo atajiona salama (secured). Mara nyingine hii itamaanisha kusimama Karibu na mwanao pale atakapokua akiongea na mgeni kwa kusudi tu la kumfanya ajihisi salama na huru kuzungumza.
Tuhitimishe hapa kwa leo. Niseme malezi ni saikolojia, vile utakavyofaulu kumlea mtoto katika mazingira chanya kisaikolojia unamuongezea fursa za kimaendeleo katika utoto wake na hata ukubwani pia.

Tuungane tena wakati mwingine. Asanteni.
Share on Google Plus

About The Light