Mwanafunzi anamuuliza mwalimu wake: “Mwalimu hivi inakuaje kwamba wewe hufundishi masomo yote, lakini unategemea mimi nifaulu masomo yote?
Kama wewe ni mwalimu, Ungefafanua vipi majibu yako kwa huyu mwanafunzi?
Weekend iliyopita nilipata fursa ya pekee sana kuwa na wasaa mzuri na marafiki, ma-kaka, ma-mentor na vijana wenzangu mahala fulani. Tulikua na muda mrefu sana wa mazungumzo yahusuyo Serikali ya Tanzania, Uchumi na sekta ya Elimu.
Brian, Martin, Bill, Rev. Lazarus kwa pamoja tulijadiliana mambo mengi sana ambayo sisi kama watanzania ni muhimu sana kuyafahamu, kuyahoji na kuhusika.
Brian (19-20 years old) alikua kiongozi wa mjadala huu na alituvutia na kutufungua mawazo wengi sana ambao tulikua katika majadiliano hayo. Brian alituambia kuhusu uzoefu wake ambao ulizidi wote tuliokuwepo pale licha ya umri wake kuwa mdogo, yeye amekua akifanya kazi na vijana wa shule za sekondari zilizopo Holili huku Mkoa wa Kilimanjaro, hususan juu ya ndoto zao kama wanafunzi na vile Taifa, Bara na Dunia kwa ujumla inawategemea sana.
Akiwa shule moja alitoa changamoto kwa wanafunzi kujihoji kwa nini wapo shule! Wengi walijibu wapo kwa sababu wanataka wawe watu fulani. Brian aliwaambia kwamba unakosea sana kuja hapa ukiwa na ndoto ya kufanywa kuwa mtu fulani! Kabla hujaja hapa ulikua na wajibu na jukumu la kujua wewe ni nani? Hii ni muhimu sana; kuna platforms nyingi sana za kukusaidia kuendeleza kile ambacho uko vizuri kwacho. Kama hujui wewe ni nani mahali gani, kazi pekee utakayoweza fanya eneo hilo ni kazi ya KUPOTEZA MUDA.
Hii ndiyo sababu kuna ambao tangu saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni wanapiga kelele darasani na kuruka juu ya madawati, tofauti na wengine ambao wanakuwa wakiwashangaa wanawezaje kufanya hivyo ilihali wao hata muda wa kusoma wanaona bado hauwatoshi. Pengine kuna mahali ungeweza ku-fit vizuri, pengine hauko sehemu sahihi. Umewahi kuwaza wapi ungekuwepo ungeweza kuwa na matumizi mazuri zaidi ya rasilimali-muda, tena bila ya shuruti?
Swala hili lilitupa upeo wa kuutazama mtaala wa elimu wa nchi za Afrika. Kuna changamoto sana katika mtaala wetu wa elimu! Si katika mambo yaliyopo ila katika mambo yasiyokuwepo. Matatizo mengi sana yaliyopo katika elimu, jamii, taasisi na maeneo mabalimbali ya kazi, chanzo kikubwa ni kutokushiba kwa mtaala unaozalisha rasilimali watu.
Mtaala wetu uko static, hata mabadiliko ambayo hutokea hupapasa tu mtaala huo na kuuacha kama ulivyo kwa asilimia zaidi ya 90%. Hii ni tofauti sana na nchi za nje ya Africa ambazo mtaala hubadilika kwa kadri ya ugunduzi, teknolojia, na mabadiliko ya jamii husika. Ni ngumu kuleta mabadiliko kwa kuwa chini ya mfumo ule ule ambao kwa miaka zaidi ya 50 haujaweza kuzalisha rasilimali watu yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za wakati husika.
Ni ngumu kukabiliana na natizo la ajira kwa nchi za Afrika, kama tutabaki na fikra ya kwamba kama hujasoma ama huna elimu ya kiwango fulani au huna alama nzuri katika masomo ya darasani huwezi kumudu changamoto za kimaisha. Yafaa tufike mahali, uchoraji, ufumaji, michezo, ucheshi, muziki vitambulike katika uzito ule ule tunaotambua taaluma nyingine. Ukipatikana mtaala ambao unatoa kipaumbele katika vipaji, sawa na kipaumbele kinachotolewa katika masomo mengine, tutatengeneza uwanja mpana wa ajira za kujitegemea na vile vile kuwa na Watanzania walioivishwa vizuri kukabiliana na anga la kimataifa katika ubora wa vipaji na utendaji.
Sababu inayowafanya wengi waseme hata kwa miaka 1000 hatutaifikia ulaya, si kwa sababu waafrika hawana uwezo wa ugunduzi na akili za kufanya mambo makuu; hapana; ila ni kwa sababu tunafikiri katika boksi lile lile kwa miaka 50, tunafanya mambo katika mfumo ule ule kwa miaka 50. Hakuna namna hali itaacha kuwa ngumu.
Haina ulazima sana wa wewe kuanza kujifunza ukandarasi ukifika miaka 20-25 wakati ulishagundua passion yako katika ukandarasi tangu ukiwa na miaka 10. Kuna namna inawezekana kujifunza vipengele vya kozi hiyo tangu mtoto akiwa darasa la tano. Kuna uwezekano wa mtu kuchagua kuacha masomo 3-5 kati ya 10-12 akiwa kidato cha kwanza kama anaona kabisa masomo hayo hayahitaji kwa kule anakoelekea.
Kuna uwezekano wa kuongeza masomo yahusuyo uvunaji wa gesi, utunzaji wa mazingira, ujasiria mali, uongozi kuanzia shule za msingi. Hii itawasaidia watoto wetu wasiwe wageni katika fursa ambazo zinahitaji ujuzi wao. Kama mtoto atagundua passion yake mapema na kuiandama tangu akiwa na umri mdogo, ni bila shaka akifikisha miaka 15-20 anao uwezo kabisa wa kutumika na kuchangia vipaji na ustadi wake katika utendaji kazi na uzalishaji.
Mabadiliko haya ni ya msingi sana. Ifike mahali mfumo uwe safi na tuwe na watu sawia katika nyadhifa mbalimbali. Dhana dunishi na fukarishi zifike mwisho. Dhana ya kwamba UALIMU, UFUNDI, MUZIKI, na nyingine zinazofanana na hizi; ni taaluma za watu ambao hawakufanya vizuri vya kutosha katika ufaulu wao wa elimu ya sekondari, ifike mwisho. Mazingira ya hizi taaluma yaboreshwe lakini pia viwekwe vigezo vya juu kwa mtu kuchaguliwa katika taaluma hizi.
Kwa kumalizia niseme; pengine mabadiliko kama haya yakahitaji muda, its OK; naamini pengine anayesoma hapa ndiye raisi ama waziri kwa miaka 20 ijayo! Au anayesoma hapa mtoto wake atakua kiongozi katika nyadhifa hizi; andaa namna yake ya kufikiri na kuichukua dunia na changamoto zake. Hakuna Changamoto iliyopo duniani ambayo mwanadamu hana jawabu lake, ni vile hajatengeneza mazingira au hajawekeza muda na uwezo wake katika kutoa majawabu hayo.
Inawezekana Afrika, Inawezekana Tanzania, Ipo nafasi ya kuanza kufanya mambo kwa utofauti na kuongeza spidi ya ukuaji wa ugunduzi, teknolojia na uchumi. Kwa makadirio ya miaka 20 kuanzia sasa endapo tutachukua risk ya kufanya mambo kiutofauti tunaweza kuishangaza dunia.
Siamini Afika hakuna kina Marcus Rashford, Kina Raheem Sterling, Kina Woodburn, na wengine wengi; wacheza mpira wadogo kabisa wenye vipaji vya kipekee, basi na tuwape fursa kuanzia mashuleni, umitashumta irejeshwe katika ubora wa wadau na wadhamini kusajili vipaji. Sitaki kuamini afrika hakuna kina Mark Zuckerberg, Kina Steve Jobs, kina Larry Page na wengineo; watu waliofanya mapinduzi makubwa kwenye ulimwengu wa mawasiliano na teknolojia. Tutoe uwanja wa watoto wetu kudadisi na kutumia muda mwingi kuharibu kwa dhumuni tu la kujifunza.
INAWEZEKANA.
WATU WA KUBADILISHA HATMA YA AFRIKA NI MIMI NA WEWE. TUANZE KUFIKIRI, KUTAZAMA NA KUYAKABILI MAMBO KATIKA JICHO LA FUTURE. SAFARI HII IMESHAANZA NA TUTAFIKA; wengine pengine tutaiona hii siku, ila wengine pengine tutakua tumeshapumnzika! Vyovyote vile JUKUMU HILI NI LETU SOTE. AFRIKA UNA KILA SABABU YA KUWA SUPER POWER.
0 comments:
Post a Comment